SERIKALI imeanza kuchukua hatua ya kudhibiti wizi unaofanywa na watendaji katika sekta mbalimbali nchini hasa kwenye upande wa utoaji huduma za afya.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alisema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Shinyanga.
Mkutano huo ulikwenda sanjari na kusimikwa kwa Makamanda wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) ngazi ya wilaya na mkoa pamoja na uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Alisema serikali imekuwa ikijitahidi kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa katika hospitali lakini wananchi wamekuwa wakilalamika kwa kutopatiwa badala yake, huelekezwa wakazinunue.
“Wananchi nawaeleza kuwa serikali imeanza kuchukua hatua ya kudhibiti wizi, sasa imepata mbinu ya dawa zinazotolewa na serikali kuwekewa nembo au alama ili kutambulika na mtu yeyote atakayebainika kuuza dawa hizo atachukuliwa hatua,” alisema Nchemba.
Aidha katika uzinduzi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa aliasa viongozi wa CCM mkoani Shinyanga kutoteua watu kwa kuangalia ushabiki na kujaza nafasi bali waangalie watu wanaofahamu Katiba ya chama na watakaofuata na kutekeleza Ilani.
Waliosimikwa ni pamoja na Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum anayekuwa Kamanda wa UVCCM wa Mkoa. Wengine ni John Sukili ambaye ni Naibu Kamanda wa Mkoa.
Elias Kwandikwa amekuwa Kamanda wa UVCCM Wilaya ya Kahama akisaidiwa na Ezekiel Maige ambaye ni Mbunge wa Msalala.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment