Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro ametoa mwito kwa
wananchi kujitokeza kwa wingi wakati wa kutoa elimu katika vyombo
vinavyosimamia haki na sheria.
Amesema hatua hiyo, itawawezesha kufahamu haki inapotendeka na
kuondoa manung’uniko, yanayotokea mara kwa mara katika vyombo hivyo.
Aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria, yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Zimamoto Manispaa ya Shinyanga.
Aliwataka kujitokeza kusikiliza elimu, inayotolewa katika makundi ya
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na
Mahakama.
“Mahakama kushirikiana na wadau wanatakiwa kupunguza kesi ikiwa
magerezani kuna malalamiko mengi na masomo ya kufahamu sheria mbalimbali
au kutembelea maeneo ya magereza yawe endelevu ili kuweza kuondoa
changamoto zilizopo hasa zinazoelezwa na wananchi,” alisema Matiro.
Ofisa Mradi wa Ulinzi wa Mtoto kutoka shirika linalojihusisha na
msaada wa kisheria (Paceshi), Shadia Nurdin aliyehudhuria maadhimisho
hayo, alisema mpaka sasa kuna kesi 40 zinazoendelea katika Mahakama ya
Wilaya hadi Mahakama Kuu na kesi 10 zimekwishatolewa hukumu, ila
zinazoongoza ni zile za masuala ya ardhi na mirathi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Sekela Mwaiseje
alisema uzinduzi wa wiki ya elimu ya sheria ni kutoa fursa kwa wananchi
kutambua haki zao kwa utaratibu ikiwemo mwenendo wa kesi za mirathi na
ardhi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Shinyanga, Rahimu Mushi alisema
wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kutotendewa haki na Mahakama,
chanzo ni wao kutokuwa na elimu, hivyo sasa wameamua kushirikisha
wananchi na wadau ili kuwapatia elimu.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment