Home » » VIGOGO 2 ACACIA WAJIUZULU WARITHI WATAJWA

VIGOGO 2 ACACIA WAJIUZULU WARITHI WATAJWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Imeandikwa na Isdory Kitunda
KAMPUNI ya Acacia imebainisha kuwa Ofi sa Mtendaji Mkuu wake, Brad Gordon na Ofi sa Mkuu wa Fedha, Andrew Wray wameachia ngazi katika nafasi hizo.
Acacia ni moja ya kampuni kubwa za uchimbaji wa madini ya dhahabu Afrika na ina migodi mitatu Kaskazini- Magharibi mwa Tanzania, ambayo ni Bulyanhulu mkoani Shinyanga, Buzwagi wilayani Kahama mkoani Shinyanga na North Mara wilayani Tarime mkoani Mara. Kampuni hiyo imetangaza kuwa wawili hao wataondoka rasmi Acacia mwishoni mwa mwaka huu.
Kuachia ngazi kwa viongozi hao wawili, kumekuja ikiwa ni takribani miezi miwili tangu kampuni hiyo ya Acacia kumaliza mgogoro wake na Serikali ya Tanzania kuhusu udanganyifu katika usafirishwaji wa makinikia ya dhahabu.
Mgogoro huo ulianza baada ya Rais John Magufuli kupiga marufuku kusafirishwa nje ya nchi kwa mchanga wa madini wa Kampuni ya Barrick kwa kile ambacho ilisema ni kuwepo kwa udanganyifu kuhusu thamani ya madini yaliyomo kwenye mchanga huo. Hata hivyo, viongozi haowawili waliojiuluzu pamoja na timu ya viongozi na watalaamu mbalimbali kutoka Tanzania wakiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Palamagamba Kabudi, walifikia makubaliano ya kumaliza mgogoro huo.
Makubaliano hayo ni pamoja na Barrick kuingia makubaliano na Serikali ya Tanzania ya kuilipa dola za Marekani milioni 300 (sawa na Sh bilioni 700) kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya kampuni hiyo.
Hata hivyo, taarifa inayopatikana kwenye tovuti ya kampuni hiyo imeeleza kuwa, Peter Geleta ataiongoza kampuni hiyo katika kipindi cha mpito huku Jaco Maritz akiongoza kitengo cha fedha. Wateule hao wataanza kazi kuanzia Januari mosi, mwakani.
Akizungumzia kujiuzulu kwa Brad na Andrew, Mwenyekiti wa Acacia, Kelvin Dushnisky amenukuliwa na taarifa hiyo akisema, “Brad na Andrew wamekuwa kiungo muhimu katika uendeshaji na masuala ya fedha hapa Acacia kwa kipindi cha zaidi ya miaka minne. Kwa niaba ya bodi, ninapenda kuwashukuru kwa mchango wao kwenye kampuni. Tunawatakia kila la heri kwa siku za usoni.”
CHANZO HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa