MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro amemsimamisha kazi
mwenyekiti wa kijiji cha Sayu, kata ya Pandagichiza, Mataifa Balekele
(54) baada ya wananchi wa kijiji kudai kuwamwenyekiti huyo amekuwa na
tabia ya kuwachungulia kwenye madirisha nyakati za usiku wakiwa
wamelala.
Matiro alikutana na madai hayo katika mkutano wa kijiji hicho jana
baada ya kufanya ziara kwa ajili ya kukagua ulimaji wa zao la pamba.
Pamoja na kumsimamisha Mkuu huyo wa wilaya alikemea vikali tabia hiyona
kusema ni utovu wa maadili.
Aidha katika mkutano Mwenyekiti wa kitongoji Paul Selena aliteuliwa
kukaimu nafasi hiyo. Mkuu huyo wa wilaya alichukua jukumu la
kumsimamisha kazi Balekele baada ya baadhi ya wananchi akiwemo Daud
Kapela kueleza kuwa mwenyekiti wao huyo amekuwa na tabia ya
kuwachungulia kwenye madirisha nyakati za usiku wakiwa wamelala na
alipobainika alikubali kosa na kulipa faini.
Akitoa ufafanuzi, mbele ya mkuu wa wilaya, Ofisa Mtendaji wa kata
hiyo Denis Kimwaga alisema uamuzi wa kumsimamisha kazi mwenyekiti huyo
ulichukuliwa tangu Oktoba mwaka huu baada ya uongozi wa serikali ya
kijiji kukaa na kujadili malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai
mwenyekiti huyo amekuwa na tabia ya kuchungulia kwenye miji yao nyakati
za usiku.
“Kikao hicho kiliridhia mwenyekiti huyo asimamishwe kazi kutokana na
tabia hiyo ya kuchungulia kwenye kaya za watu wakiwa wamelala huku yeye
mwenyewe akikiri kufanya vitendo hivyo akidai kuwa amepitiwa tu na
shetani na kuomba kuwalipa fedha kama fidia watu aliowachungulia,”
alieleza Kimwaga.
Hata hivyo, Balekele akizungumza kwa njia ya simu, kwa kuwa hakuwepo
mkutanoni alieleza kukubaliana na uamuzi uliofikiwa wa kusimamishwa huku
akikataa kujihusisha na tabia ya kuchungulia watu akidai kuwa tuhuma
hizo ni chuki binafsi.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ambao hawakutaka kutaja majina yao
walisema kuwa mwenyekiti huyo alikuwa amewachosha na tabia zake. “Huyu
ni mtu mzima tena kiongozi ambaye ameonesha tabia mbaya, kwani ana
familia inayomtegemea kama mke na watoto pamoja na wajukuu imekuwa ni
tabia yake ya muda mrefu, amechungulia katika kaya nyingi ambazo wenyewe
hawataki kujionesha ni aibu sasa tumechoka kuchunguliwa,” alisema mkazi
mmoja wa kijiji hicho.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment