SABABU ya wanawake kuongoza kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
(VVU) inatokana na kukosa maamuzi juu ya kutumia kinga kama kondom
wanapofanya tendo la ndoa.
Hayo yalibainishwa wilayani hapa jana na Mwezeshaji Kaskile Jumanne
katika semina iliyoandaliwa na Shirika la The Foundation for Human
Health Society (HUHESO) inayotekeleza mradi wa kuwakomboa wasichana
wanaofanya biashara ya ngono, unaofadhiliwa na Rapid Funding Envelop (RFE) ya jijini Dar es Salaam.
Jumanne ambaye ni Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, alisema
wanawake huathiriwa na mfumo dume wa kukosa maamuzi katika tendo la
ndoa jambo ambalo huchangia wakipata maambukizi kwa urahisi.
Alibainisha kuwa kwa jamii ambayo ni muumini mzuri wa kutumia kondomu
lakini baadhi ya watu pia hujikuta wakipata maambukizi mapya kutokana
na kutofahamu matumizi sahihi wakati wa kuvaa, kuivua na kuhifadhi
baada ya matumizi.
Mkurugenzi wa HUHESO, Juma Mwesigwa alisema wanawake wanapaswa
kubadilika na kuondokana na jukumu la mapenzi kutawaliwa na mwanaume
ili kuondokana na hatari ya kupata maambukizi mapya.
Mwesigwa alisema wanawake hawana budi kujitambua kwa kubadilika na kuwa jasiri jambo litakalosaidia kupunguza maambukizi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment